Follow us:

Press Release in Kiswahili: The National Launch of ALIVE Report, Tanzania

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

 

Dar es Salaam, 24th January 2023

 Je, watoto wetu wa Tanzania wanazo stadi za maisha na maadili?

Takwimu zinaonesha kuwa, kwa Tanzania-bara vijana wengi wenye umri  kati ya miaka 13 – 17 , wana kiwango cha chini cha stadi za maisha(LifeSkills). Kwa Mfano ni asilimia 8 tu ya vijana wana uwezo wa utatuzi wa matatizo, yaani, wanaweza kutambua kuwepo kwa tatizo kutoka kwa mitazamo tofauti tofauti, wakielewa kuwa kunaweza kuwa na njia nyingi na kuchagua iliyobora (Kiwango cha juu cha utatuzi wa matatizo ). Hii ni moja kati ya matokeo ambayo yanatarajiwa kutolewa wakati wa uzinduzi wa ripoti ya tathmini ya kaya ya ALiVE-Tanzania, utakaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, Tarehe 26 January, 2023.  

Kwa kutilia mkazo, stadi za maisha na tunu zinatambuliwa kuwa ni sehemu ya msingi ya elimu kwani huongeza uwezo wa kujifunza kwa wanafunzi.  Pia kwa upande wa ajira,  waajiri nao  wanazingatia zaidi umahiri wa stadi za maisha na maadili kama vile utatuzi wa matatizo, ubunifu, mawasiliano, fikra tunduizi, ushirikiano, kujitambua na stadi nyinginezo ili kuongeza ufanisi katika kazi.

Kwa kutambua hilo mwaka 2005, Tanzania ilianzisha mtaala unaozingatia umahiri (competence based curriculum) ili kusawazisha mapungufu ya mtaala uliopita ambao haukuwawezesha wahitimu kuwa na umahiri unao hitajika katika soko jipya la ajira. Wakati hili linatendeka, walimu wengi na wazazi wengi hawakuwa na uelewa juu ya umuhimu wa umahiri huu. Pia hakuna ushahidi wowote wa kuonesha kuwa watoto wetu  wanajifunza au hawajifunzi  umahiri huu  wakiwa shuleni au nyumbani.

Pamoja na ukweli kwamba watu wengi wanakubaliana kwamba stadi za maisha ni muhimu, hakuna ushahidi wa kutosha unaotoa taswira ya kiwango cha umahiri wa watoto katika stadi za maisha na maadili, zaidi ya matokeo ya kitaaluma.

Tumeweza kufanya kwa mara ya kwanza tathmini ya kitaifa ya stadi za maisha na maadili kwa vijana na kupata matokeo. Hivyobasi, ni wakati maridhawa kujikita katika mijadala chanya kuhusu nini tutaweza kufanya ili kuwajenga watoto wa Tanzania katika stadi hizi kupitia mfumo wa elimu na malezi nyumbani.

“Tunatarajia ripoti hii ya kipee kabisa kuwahi kutolewa Tanzania, na Afrika Mashariki, itachochea mijadala chanya kuhusu umuhimu wa stadi za maisha na nini kifanyike kuhusu ujifunzaji wa watoto wetu ili kuwasaidia kujenga stadi hizi.” Anasema Bw. Samson Sitta – Mratibu wa Mradi wa ALIVE – Tanzania kutoka Shirika la Milele Zanzibar Foundation

Aidha, aliongeza kwamba, “Tunakwenda kufanya Uzindizi wa ripoti hii siku ya Alhamisi, Tarehe 26 Januari 2023, katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam; ambapo viongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia; wadau mbalimbali wa Elimu wa Tanzania, Afrika Mashariki na Duniani watahudhuria”.

Tathmini ya ALiVE imefanyika katika wilaya 34 ndani ya mikoa 18 ya Tanzania Bara, kati ya mwezi Juni – Septemba 2022. Jumla ya vijana 14,645 wenye umri wa miaka 13-17 walifanyiwa tathmini/upimaji huo kutoka katika kaya 11,802.

Kuhusu Mradi wa Tathmini ya Stadi za Maisha na Maadili Afrika Mashariki (ALiVE)

ALiVE ipo chini ya Mtandao wa Kikanda wa Elimu na Ujifunzaji  (Regional Education Learning Initiatives-RELI), kupitia kongani ya maadili na stadi za maisha (VALi) hii inaratibiwa na Zizi Afrique Foundation NGO iliyoko nchini Kenya, Luigi Giussani Taasisi ya Elimu ya Juu nchini Uganda na  Milele Zanzibar Foundation kwa Tanzania. Aidha tathmini ya ALiVE kwa Tanzania bara ilifanywa kwa Ushirikiano wa mashirika mawili; Milele Zanzibar Foundation na Uwezo Tanzania.

Tafadhali jisajili sasa kupitia https://rb.gy/4uijoa ili kuweza kujiunga katika uzinduzi huo.

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasialiana na 

 Mratibu wa Mradi wa ALiVE,Tanzania. Samson Sitta|sjohn@mzfn.org|+255710155 303| http://www.mzfn.org

Open chat
1
Hello!
Can I help you